VODACOM YATOLEA UFAFANUZI KUHUSU THAMANI YA HISA ZAKE

Dar es Salaam April 20, 2017: kumekuwa na taarifa za upotoshaji, hasa katika mitandao ya kieletroniki ya kijamii, kuhusu thamani halisi ya hisa za Kampuni ya Vodacom Tanzania Plc (VTL) ambazo zinauzwa kwa umma hivi sasa.
Kumekuwa na ujumbe mfupi uliozungushwa tarehe 19 Aprili, 2017  ukionyesha kuwa thamani halisi ya Kampuni hiyo ni pungufu sana ya ile inayoashiriwa na bei ambayo hisa zake zinauzwa.

Umma unatakiwa kufahamu kuwa  ukokotoaji wa thamani ya hisa zinazouzwa umezingatia viwango vya kitaalamu vya kimataifa.

Kama ilivyoainishwa kwenye kipengele 2.1 cha Waraka wa Matarajio, bei ya TZS 850 kwa hisa umepitishwa na Wakurugenzi wa VTL kwa kuzingatia ukokotoaji na mapendekezo ya Mshauri Kiongozi, uliofanywa kwa kuzingatia mwenendo wa uchumi wa Nchi, historia  na mwelekeo wa biashara na faida wa Kampuni, na mwenendo wa bei za hisa za makanpuni yanayoshabihiana na VTL katika masoko mengine ya Afrika hususani Kenya (Safaricom), Morocco (Marroctel) na Africa Kusini (Vodacom Group Plc.).

Ukokotoaji wa thamani ulizingatia nguvu ya kibiashara ya Vodacom katika upeo wa kati na mrefu ambapo Wakurugenzi wanaamini Kampuni inaweza kujiimarisha zaidi kutokana na mwenendo wake katika siku zilizopita, kuisha kwa changamoto ilizopitia katika miaka ya karibuni, ongezeko la mapato linalotokana na kupanuka kwa biashara zake katika nusu ya pili ya mwaka 2017 (ulioishia tarehe 31 Machi, 2017), pamoja na uwekezaji uliofanyika na unaokusudiwa kufanywa. Matokeo ya ukokotoaji yalilinganishwa na mwenendo wa bei za kampuni zinazofanya biashara kama ya Vodacom katika masoko mengine kama ilivyotajwa hapo juu, baada ya kuzingatia tofauti za ukubwa wa soko na hali ya uchumi jumla.

Kwa kuzingatia matokeo ya uchambuzi huu, bei ya TZS 850 kwa hisa imefikiwa baada ya kugawanya thamani ya mtaji wa VTL kwa kiasi cha hisa kilichokwisha kutolewa.
Haihitaji utaalamu mkubwa wa masuala ya masoko ya mitaji kugundua upungufu ulio katika ujumbe mfupi uliosambazwa tarehe 19 Aprili, 2017.

Ujumbe huo unadai kuwa njia ya kufahamu thamani ya kampuni ni kukokotoa thamani ya rasilimali za kampuni baada ya kutoa dhima (Net Asset Value – NAV). Njia hii si sahihi kutumika kwa ajili ya kukokotoa thamani ya kampuni inayoendelea na biashara (yaani going concern), bali hutumika kwa kampuni inayofungwa (kufilisiwa) kwa lengo la kufahamu uwezo wa kulipa madeni yake.
Tofauti na kampuni inayofungwa ambapo hakuna hitaji la kuzingatia uzalishaji wa mapato ya siku zijazo, uthamani wa  kampuni inayoendelea na bishara unazingatia zaidi uwezo wa kuzalisha mapato katika muda ujao. Kwa hiyo, ni kawaida thamani ya kampuni kuwa kubwa kuliko thamani ya vitabuni ya rasilimali za kampuni husika baada ya kutoa dhima.

Kwa mfano, wakati ujumbe mfupi uliosambazwa unadai kuwa bei ya hisa za VTL ambayo ni takribni mara 3.8 ya thamani ya rasilimali zake baada ya kutoa dhima ni ushahidi wa udanganyifu, hisa za Safaricom nchini Kenya ziliuzwa kwa bei ambayo ni mara 5.8 zaidi ya thamani ya vitabuni ya rasilimali za kampuni hiyo baada ya kutoa dhima kwa mujibu wa taarifa ya soko la hisa la Nairobi ya tarehe 18 Aprili, 2017. 
Hii inaonyesha siyo tu makosa yaliyobebwa na ujumbe huo mfupi bali pia upungufu mkubwa wa ufahamu wa masuala ya uthamanishaji wa biashara na hisa za makampuni alionao mwandishi wake.

wawekezaji kuzingatia ushauri wa nguli wa uwekezaji katika masoko ya hisa, Warren Buffet wa Marekani, kuwa:'Ni bora kununua kampuni ya bora kwa bei ya haki kuliko kununua kampuni ya wastani kwa bei ya chini.' 

Wawekezaji tarajiwa mnaaswa kupuuza ujumbe huo wa kupotosha na usio wa kitaalamu.
Share on Google Plus

About Unknown

2 comments:

  1. Pamoja na hayo tuongezee muda WS kununua hisa.Kama mwezi zaidi

    ReplyDelete
  2. Pamoja na hayo tuongezee muda WS kununua hisa.Kama mwezi zaidi

    ReplyDelete