MBUNGE WA SINGIDA MASHARIKI TUNDU LISSU APEWA USHAURI NA SERIKALI

Serikali imemshauri Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu kutekeleza wajibu wake kwa kusimamia weledi akiwa kama Wakili wa Mahakama Kuu badala ya kufanya Propaganda kwa kutumia lugha ya kejeli, kuudhi na uchochezi kuituhumnu Serikali kuwa inabana demokrasia.
Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi leo July 18 2017.
“Vyombo mbalimbali vya habari leo vimemnukuu Mbunge wa Singida Mashariki Ndugu Tundu Lissu ambapo pamoja na mambo mengine, huku wakati fulani akitumia lugha za kuudhi, uchochezi na kejeli, ameituhumu Serikali kuwa inabana demokrasia nchini,” imefafanua taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imesema kuwa madai kwamba Serikali inakandamiza demokrasia ni propaganda tu za kisiasa, kutokana na Lissu kuonekana kuchanganya kati ya haki katika demokrasia ambazo hata yeye amezitumia kuongea na wanahabari bila tashtiti kwa upande mmoja na misingi ya wajibu kwa upande mwingine ambayo kila mmoja, iwe Tanzania au kwingineko duniani, anayo na pale anapoikiuka hatua huchukuliwa.
Dkt. Abbasi amesema kuwa tofauti na upotoshaji wa Lissu, Tanzania ikiwa nchi kiongozi Afrika na duniani katika kuenzi demokrasia na kupigania haki, si tu inaendelea kuenzi misingi hiyo bali pia imechukua hatua za wazi kuhakikisha kuwa misingi hiyo inalindwa na pale mtu na hata taasisi zinapokiuka basi mkondo wa sheria, jambo muhimu katika utawala bora, huchukua nafasi yake.
Vilevile ameeleza kuwa, Tanzania ni ikiwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) imeridhia mkataba wa Kimataifa wa haki za kiraia na kisiasa wa mwaka 1966 na huwasilisha taarifa zake za utekelezaji wa demokrasia na haki za binadamu katika kamisheni ya UN ya haki za binadamu.
Pia ni mwanachama kiongozi wa Umoja wa Afrika (AU) ambapo imeridhia Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu na ni miongoni mwa nchi za kwanza kabisa Afrika kukubali kushtakiwa na wananchi wake kwa kuridhia itifaki ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na pia kukubali kufanyiwa ukaguzi katika utawala bora kupitia Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).
“Ni kwa sababu hizi basi tunamuasa Ndugu Lissu na wananchi kwa ujumla kujiepusha na propaganda, kejeli na uzushi usio na msingi dhidi ya Serikali au taasisi zake na pale ambapo wanadhani kuna haki zimekiukwa badala ya kuvunja sheria ni vyema kutafuta haki kupitia mkondo wa kisheria ambao tumeuainisha hapo juu,” imefafanua taarifa hiyo.
Dkt. Abbasi amesema kuwa Serikali itaendelea kuenzi na kuilinda misingi ya demokrasia, uhuru wa watu na kuwapa fursa wananchi kushiriki katika uchumi wa nchi hasa wakati huu wa mageuzi makubwa ya kiutendaji chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli lakini haitavumilia mtu yeyote au kikundi chochote kitakachojaribu kutumia uhuru wowote vibaya ili tu kukwaza azma hiyo ya Taifa.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment