VITUO VYA MAFUTA ZAIDI YA 160 VYAFUNGIWA KWA KUSHINDWA KUTOA RISITI ZA EFD

Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA imevifungia Zaidi ya vituo 154 nchi nzima kufuatia zoezi la ukaguzi wa matumizi wa mashine za kutolea risiti za EFD katika vituo vya kuuzia mafuta linaloendelea nchi nzima.
TRA jana ilivifunga jumla ya vituo 20 vya kuuzia mafuta katika jiji la Dar es Salaam huku vituo 72 kati ya 80 vilivyokaguliwa Kanda ya Ziwa vikifungwa, ambapo vituo nane tu ndivyo vilivyokidhi kigezo cha kuwa na mashine za EFD za kutolea risiti moja kwa moja wakati wa mauzo. Naye Meneja wa TRA Mkoa, wa Arusha, Akili Mbaruk alithibitisha kuvifungia vituo 54 vya mafuta baada ya kushindwa kutoa risiti za EFDn huku mkoa wa Dodoma ukiripoti kuvifungia vituo 8.
Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere jijini Dar es salaam alivifungua vituo vitatu tu kati ya 20 vilivyofungiwa jijini Dar es salaam baada ya kukamilisha kigezo cha kuwa na mashine za kutolea risiti kwenye mashine za mafuta.

Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere akifungua moja kati ya vituo vitatu vya mafuta vilivyokidhi masharti ya kuwa na mashine ya kutolea risiti ya EFD

Akizungumza mara baada ya kufungua vituo hivyo, Kamishina wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere amewashukuru wamiliki wa vituo hivyo kwa kuonyesha ushirikiano kwa serikali kwa kutimiza masharti waliyopewa ya kufunga mashine hizo na kusisitiza kuwa hakuna kituo kitakachofunguliwa kama hakitatimiza masharti.
“Niwaombe wamiliki wa vituo vilivyofungiwa kuwa kwa sasa hakuna kitakachofunguliwa bila kutimiza mashart, timiza masharti tuje tukague na tukufungulie uanze biashara yako,” amesema Kamishna Kichere.
Amesema vituo vilivyofunguliwa jana ni pamoja na GBP kilichopo eneo la Majumba Sita, Simba Oil kilichopo eneo la Sitakishari, Ukonga na PETRO kilichopo eneo la Kigamboni.
“Kitendo cha kuunganisha mashine hizi na pampu za mafuta ni cha muda mfupi sana na wala hakichukui muda mrefu, angalia huyu tulimfungia siku ya jumanne tarehe 11 Julai na leo Ijumaa Julai 14 ameshafunga mashine na anaanza kufanya biashara bila kugombana na serikali;” amesema Kamishna Kichere.
Zoezi hilo bado linaendelea nchi nzima huku waathirika wakiwa ni madereva, abiria na watumiaji wengine wa vyombo vinavyotumia mafuta. Serikali ilitoa agizo hilo la kuwataka wateja wanaonunua mafuta kudai risiti pindi wanaponunua bidhaa hiyo kutoka kwenye vituo vya kuuzia mafuta huku vituo hivyo vikilazimika kufunga mashine za kutolea risiti (Automatic EFD).
Baadhi ya madereva wakisubiri mafuta katika kituo kimoja jijini Dar es Salaam






Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment