TUME YA UCHAGUZI TANZANIA IMETAJA TAREHE YA MARUDIO YA UCHAGUZI



Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 43 kuwa utafanyika Novemba 26 mwaka huu. Mwenyekiti wa NEC Jaji Semistocles Kaijage, amesema kuwa uchaguzi huo unafanyika kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo baadhi ya madiwani kufariki dunia, kujiuzulu, kutohudhuria vikao na wengine ushindi wao kutenguliwa na Mahakama. 

Jaji Kaijage amesema tume imetangaza kufanyika kwa uchaguzi huo mdogo, baada ya waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa kuitaarifu tume uwepo wa nafasi wazi za madiwani katika kata hizo 43 zilizoko katika halmashauri mbalimbali 36 na mikoa 19 ya Tanzania Bara.
Jaji Kaijage ameainisha kwamba kifungu cha 13 (1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya. 292 kinampa mamlaka waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kuitarifu tume kuhusu kuwepo kwa uchaguzi huo mdogo wa madiwani.
Amefafanua kuwa baada ya kupokea taarifa hiyo na kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa; Sura ya 292, Tume ya taifa ya uchaguzi ina wajibu wa kuitisha na kuendesha Uchaguzi mdogo katika Kata hizo.
“Hivyo, ninapenda kuchukua nafasi hii kutoa taarifa kuwa tume imepanga kuendesha uchaguzi mdogo katika Kata 43 tarehe 26 Novemba, 2017,” alisema Jaji Kaijage.
Amesema ratiba ya mchakato wa uchaguzi huo itaanza Oktoba 26 ambapo kutafanyika uteuzi wa wagombea udiwani na kampeni za uchaguzi huo mdogo zitaanza Oktoba 27 na kumalizika Novemba 25.



Jaji Kaijage aliema Vyama vya Siasa, Wadau wote wa Uchaguzi na Wananchi wanakaribishwa kwa ajili ya kushiriki kwenye uchaguzi huo utakaozingatia ratiba iliyoainishwa hapo juu.
Alitoa mwito kwa vyama vya Siasa na Wadau wote wa Uchaguzi kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Madiwani) za mwaka 2015, Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 pamoja na maelekezo yote yaliyotolewa au yatakayotolewa na Tume wakati wote wa Uchaguzi mdogo.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment