KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeshindwa kutinga kwenye raundi ya mwisho ya mtoano ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufungwa na Mbabane Swallows mabao 3-0 jana jioni katika mchezo wa marudiano uliofanyika Uwanja wa Taifa wa Somhlolo, Swaziland.
Kwa ushindi huo wa Swallows, unaifanya kufuzu
kwa raundi ijayo kwa jumla ya mabao 3-1 kufuatia ushindi wa bao 1-0 iliyoupata
Azam FC katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar
es Salaam.
Kabla ya kuanza mchezo huo, wakati kikosi cha
Azam FC kikiwasili uwanjani, mashabiki wa Mbabane kwa kushirikiana na polisi wa
Swaziland walishirikiana kuifanyia vurugu timu hiyo kwa kuizuia isiteremke
ndani ya basi.
Hali hiyo ilisababisha Ofisa Mtendaji Mkuu wa
Azam FC, Saad Kawemba, kusukumwa, kupigwa na kuangushwa na polisi pamoja na
mashabiki hao wakati akijaribu kupigania haki ya Azam FC kwa kushirikiana na
maofisa usalama walioongozana na timu hiyo.
Maofisa usalama wa Azam FC waliokabiliana na
mashabiki kuzima vurugu hizo waliongozwa na Kondo Idd almaarufu kama Karume,
Juma Mdunguma, Kheri Mzozo, Edward Msimbe na Biggie Papa.
Katika hatua nyingine, Azam FC ililazimika
kutoingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo baada ya kupuliziwa dawa kali,
hali iliyoilazimu kubadilisha nguo kwenye basi za kuvaa katika njia ya kuingia
vyumbani.
Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC
kitaanza rasmu safari ya kurejea Tanzania kesho Jumatatu saa 6.15 kikiondoka
katika Uwanja wa Ndege ya Kimataifa wa OR Tambo nchini Afrika Kusini kikipitia
nchini Kenya kabla ya kutua jijini Dar es Salaam saa 3.00 usiku.
0 comments:
Post a Comment