Kocha wa timu
ya taifa ya Tanzania “Taifa Stars” leo atakuwa na jaribio jingine la kuwakabili
Burundi ‘Intamba Murugamba’ katika mchezo wa kimataifa wa Kirafiki uliopo
kwenye kalenda ya FIFA.
Mchezo huo utakuwa ni wa Pili kwa kocha Mayanga ambaye Jumamosi
iliyopita alianza vizuri kibarua chake kwa kuifunga Botswana mabao 2-0 kwenye
mechi ya Kirafiki.
Burundi tayari wamewasili Dar es Salaam jumapili mchana wakiwa
na kikosi chao kamili kikiongizwa na Mshambuliaji wa Simba Laudit Mavugo.
Kocha Mayanga katika mchezo wake wa leo atakosa huduma ya
Mshambuliaji wake Mbwana Samatta anayoichezea KRC Genk ya Ubelgiji ambaye
alifunga mabao yote mawili kwenye mchezo uliopita.
Mayanga amesema amemruhusu Samatta kuondoka ili kutumia kikosi
chake cha wachezaji wanacheza ligi ya ndani, lengo ni kuiandaa timu ambayo
itashiriki fainali za CHAN ambazo zinashirikisha wachezaji wanaocheza ligi za
ndani kwao.
Mayanga amesema maandalizi yote kuelekea mchezo wa kesho
yamekamilika na anatarajia kupata ushindi mwingine kutokana na uelewano mzuri
waliokuwa nao wachezaji wake.
“Najua utakuwa mchezo mzuri wenye ushindani kwa kuwa Burundi ni
majirani zetu, tunajuana lakini naamini tutashinda kutokana na maandalizi
mazuri tuliyokuwa nayo kuelekea mchezo huo,” amesema Mayanga.
Kocha huyo amesema kutokuwepo kwa Samatta kwenye mchezo huo
hakutaiathiri timu yake kwani kuna wachezaji wengi ambao wanaweza kucheza
nafasi yake.
Amesema kwenye nafasi hiyo anaweza kumtumia Abrahmani Mussa wa
Ruvu Shooting kucheza sambamba na Ibrahim Ajibu na anaamini atafanya vizuri
kutokana na uwezo aliokuwa nao mchezaji huyo.
Amesema kama ilivyokuwa kwenye mchezo uliopita mchezo wa kesho
atatumia mfumo ule ule wa 4-4-2 kwa sababu wanataka kushambulia zaidi na
kufunga mabao mengi.
Nahodha wa Burundi Mavugo amesema mchezo wa kesho utakuwa mgumu
kwa sababu Tanzania wanakikosi imara ambacho kinaundwa na wachezaji wengi
vijana lakini ameahidi kupata ushindi kwenye mchezo huo.
“Tumekuja tukiwa na kikosi imara ambacho kina wachezaji wengi
wenye uzoefu kwa hiyo pamoja na kucheza ugenini lakini naamini tutafanya
vizuri,” amesema Mavugo.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa mwaka 2014 uwanja wa
Taifa Dar es Salaam na Tanzania kufungwa mabao 3-1.
0 comments:
Post a Comment