IVANKA TRUMP |
Mtoto wa rais
wa Marekani Ivanka Trump amejiunga rasmi na serikali ya baba yake ambapo
atahudumu kama msaidizi wa Rais bila ya malipo yoyote, kwa mujibu wa ikulu ya
White House ambapo mumewe, Jared Kushner, ni mshauri mwandamizi
wa Rais Donald Trump.
Binti huyo wa rais wa Marekani amekubali shinikizo baada ya
wataalamu kuhusu maadili kukosoa mpango wake wa awali wa kutaka kuhudumu katika
wadhifa usio rasmi.
Bi Trump, 35, amesema amesikia "maswali ambayo baadhi ya
watu wamekuwa wakiuliza kuhusu hatua yangu kumshauri rais katika nafasi yangu
kama mtu binafsi".
Kupitia taarifa, White House imesema ina furaha kwamba
"Ivanka Trump amechukua hatua hii isiyotarajiwa katika nafasi yake kama binti
wa rais".
Bi Trump alisema kupitia taarifa yake kwamba amekuwa akifanya
kazi "kwa nia jema na kundi la washauri wa rais White House pamoja na
mshauri wake binafsi kujadili kuhusu jukumu lake".
Wataalamu kuhusu maadili walilalamika ilipobainika wiki iliyopita
kwamba Bi Trump angepewa afisi White House pamoja na kibali cha usalama cha
kuingia na kuondoka ikulu hiyo, bila yeye kujiunga rasmi na wahudumu wa rais.
Wakosoaji walisema kazi ya Bi Trump inafaa kufanywa rasmi ndipo
aweze kudhibitiwa na sheria kuhusu uwazi wa maafisa wa serikali pamoja na
maadili. Aidha, adhibitiwe na sheria kuhusu mgongano wa maslahi.
Wakili wa Bi Trump, Jamie Gorelick, amesema mteja wake
atawasilisha nyaraka zifaazo za kufichua utajiri wake kwa mujibu wa sheria
kuhusu maadili ya watumishi wa umma Marekani.
0 comments:
Post a Comment