Kero ya
uhaba wa maji iliyokuwa ikiwakabili wananchi zaidi ya 1000 wa vitongoji vitano
vya Kijiji cha Kasololo wilayani Misungwi mkoani Mwanza na kusababisha ndoa
nyingi kuvunjika pamoja na migogoro kwenye familia, imetatuliwa baada ya
Taasisi ya The Desk & Chair Foundation kuchimba na kujenga visima saba.
Mwenyekiti
wa The Desk & Chair Foundation tawi la Tanzania Sibtain Meghjee akikabidhi
visima hivyo vilivyogharimu sh 21 milioni alisema walisitisha ujenzi wa Msikiti
(nyumba ya ibada ) ili watatue kero ya maji kwa kuwapa wananchi huduma ya maji
itakayowanufaisha watu zaidi ya 1200 kwa matumizi ya kibinadamu.
Alisema
visima vimekabidhiwa ili kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Bi. Fatma AS. mjukuu
wa Mtume Mohamed S.A.W.ambaye alifanya kazi kubwa ya kusaidia jamii lakini pia
miradi ya kijamii inayofadhiliwa na waumini wa madhahebu ya Shia Ithna Asheri,
kwenye maadhimisho hayo ilikabidhiwa huko Kwimba Mwanza na Kondoa mkoani Dodoma
na maeneo mengine nchini.
“Dini ya
Kiislamu licha ya kupakaziwa mambo ya ovyo na kuhusishwa na ugaidi ni nzuri na
haya yanayofanywa na The Desk & Chair Foundation ndiyo uislamu
wenyewe.Tumewapunguzia kero ya maji wananchi wa Kasololo na siri ya kudumu kwa
visima hivi matunzo ni muhimu lakini pia tengeni maeneo yasiyo na migogoro kwa
ujenzi wa maombi mapya ya visima,”alisema Sibtain.
Wakizungumza
jana baada ya kukabidhiwa visima hivyo saba vya maji safi na salama
vilivyochimbwa katika vitongoji vitano vya vya Isuka, Bugumo,
Mwashileko,Iwelimo na Kasololo baadhi ya wananchi walisema tatizo hilo la
ukosefu wa maji lilikuwa linawakabili kwa muda mrefu litapungua ingawa bado
changamoto ipo.
Petro Mbogo
mkazi wa kitongoji cha Iwelimo kilichopata visima vitatu alisema kero ya maji
ilisababisha migongano kwenye jamii, migogoro katika familia pamoja na ndoa
nyingi kuvunjika kutokana na akina mama kukesha wakisubiri kuteka maji usiku
kwenye vyanzo vya asili ambavyo hukauka wakati wa kiangazi.
“Maji
yalikuwa kero kwa miaka mingi katika kijiji chetu na wakati wa kiangazi
tulisafiri umbali wa km 5 kwenda kuchota maji ziwani.Wanawake walikuwa
wakisumbuka mno kupata maji, ndoa nyingi zilivunjika, kulizuka migongano na
migogoro kwenye familia sababu ya maji,”alisema Mbogo.
Alisema
kupatikana kwa visima hivyo sasa kutawapa wanawake fursa na muda wa kufanya
shuguli za uzalishaji pamoja na maendeleo tofauti na zamani ambapo walipoteza
muda mwingi wakitafuta maji kwa matumizi ya familia zao na kushindwa kuzalisha.
Naye
Mariamu Jeremiah wa kitongoji cha Bugumo alisema visima hivyo vitakidhi
mahitaji ya wananchi wa vitongoji vya kijiji hicho ambao awali walifikia hatua
ya kupigana wakigombea kuchota maji kutoka kwenye visima vya asili kwa kulowa
maji (kuchota kwa kutumia kamba) huku wakilazimika kuwaacha waume zao wamelala
kwenda kutafuta maji.
“Mungu
amesikia kilio chetu cha maji japo pump ni nzito kwa watu wa umri mkubwa,tunashukuru
kwa msaada huu wa visima vya maji, maana hatukuwa tunaoga wala kufua nguo za
waume zetu, ndoa zilivunjika wanawake wengine walipigwa na waume zao kwa
kuchelewa sababu ya maji,watoto walikatishwa masomo,walikuwa hawanawi
nyuso,”alisema Bi. Jeremiah.
Alidai
walilazimika kuyafuata maji ziwani umbali wa maili 5 kutokana na kuambulia ndoo
moja kwenye kisima wakichukua muda wa saa 8 kuipata huku ndoo moja ya ujazo wa
lita 18 wakiuziwa sh.500 hali ambayo kwa wananchi wasiokuwa na ajira yalikuwa
ni mateso kumudu gharama za maji kwa familia.
Kwa mujibu
wa wakazi wa kitongoji cha Iwelimo Susan Fustine,Rahel Yuda,Shoma Motomkali na
Regina Joseph licha ya kusogezewa karibu huduma hiyo bado wanakabiliwa na adha
kubwa ya maji na hivyo waongezewe visima vingine huku Mwalimu Mkuu msaidizi wa
Shule ya Sekondari Kasololo Rahim Ayoub akieleza kuwa walimu na wanafunzi
watayatumia maji hayo kwa mahitaji ya kibinadamu na kumwagilia miti ili
kuboresha na kutunza mazingira ya shule.
Mwenyekiti
wa Kijiji cha Kasololo Ruben Masasi licha ya kushukuru kwa msaada huo ambao
haukutegemewa alidai umeondoa migogoro kwenye familia zilizokumbwa na kadhia
hiyo na kunusuru ndoa zisiendelee kuvunjika lakini kutokanana idadi ya ongezeko
la watu,mahitaji yataongezeka na kuomba wasaidiwe visima vingine.
Wananchi
wakimsikiliza mfadhili aliyechimba visima vya maji Sibatin Meghjee Mwenyekiti
The Desk & Chair Foundation ili kukabiliana na kero ya maji kijijini
Kasololo Misungwi hivi karibuni.
|
0 comments:
Post a Comment