Serikali
imesema haitavumilia wala kusita kumchukulia hatua yeyote anayevamia na kujenga
katika hifadhi za miundombinu ya barabara na reli kwani kufanya hivyo ni kosa
kisheria.
Akizungumza
na waandishi wa habari wilayani Karagwe, mkoani Kagera mara baada ya kukagua
barabara ya Kyaka hadi Bugene yenye urefu wa kilometa 59.1, Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka wananchi kuacha dhana
ya kuingilia miundombinu hiyo kwa imani ya kulipwa fidia na Serikali.
“Najua bado
kuna watu wanaendelea kuvamia miundombinu ya usafirishaji, sasa nasema kuwa
Serikali itaendelea kubomoa pasipo kulipa fidia kwa yeyote anayevunja sheria”,
amesema Profesa Mbarawa.
Kuhusu
mradi wa ujenzi wa barabara hiyo, Waziri Profesa Mbarawa amekipongeza Kitengo
maalum cha Wahandisi Washauri Wazawa (TECU), kinachosimamiwa na Wakala wa
Barabara nchini (TANROADS), kwa kusimamia ujenzi wa barabara hiyo kwa
kuzingatia viwango na kuwataka kuendelea kuimarisha kitengo hicho ili kiweze
kufikia hatua ya kujenga barabara nchini.
Aidha,
amewataka viongozi wa wilaya hiyo kuwahamasisha wananchi wake kuilinda na
kuitunza barabara hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu kama ilivyokusudiwa.
Kwa upande
wake, Mhandisi Mshauri wa mradi huo Eng. Mushubira Kamuhabwa, amesema kuwa kazi
inaendelea vizuri kwani mpaka sasa mradi huo umefika asilimia 98 ambapo kazi
iliyobaki ni uwekaji wa alama za barabarani.
Eng.
Kamuhabwa ameongeza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha
usafirishaji wa mizigo na abiria kutokana na barabara hiyo kuwa kiungo kati ya
Tanzania na nchi jirani za Uganda, Rwanda na Burundi.
Mradi wa
ujenzi wa barabara ya Kyaka hadi Bugene umejengwa na kampuni ya CHICO kutoka
nchini China na kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 64.96.
Katika
hatua nyengine Waziri Mbarawa ametembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa
shule ya Sekondari ya wavulana ya Ihungo mkoani Kagera iliyoharibiwa na
tetemeko la ardhi takriban miezi sita iliyopita.
Akiwa
katika shule hiyo Profesa Mbarawa ameridhishwa na kasi ya mkandarasi anayejenga
shule hiyo na kusema nia ya Serikali ni kuijenga shule hiyo kwa ubora wa hali
ya juu ili kukabiliana na majanga mbalimbali.
Naye, Mkuu
wa Wilaya ya Bukoba, Bw. Deodatus Kinawiro pamoja na mambo mengine ameishukuru
Serikali kwa kuwajali wananchi wake na kuijenga shule hiyo kwa ubora wa hali ya
juu.
Ni
takribani miezi sita tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi mkoani Kagera na
kuharibu miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara, madaraja, hospitali, shule
pamoja na makazi ya watu.
Kutokana na
uharibifu huo Serikali pamoja na wadau mbalimbali ilianza juhudi za ukarabati
na ujenzi wa miundombinu hiyo.
0 comments:
Post a Comment