Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani Alhaji Majid Mwanga
kuwasaka, kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wafugaji wote
wanaodaiwa kuhusika katika matukio ya kuwashambulia kwa viboko wananchi wa
Kijiji cha Fukayosi kilichopo Wilayani humo.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo Ijumaa hii alipokuwa akisafiri kwa gari kutoka Dodoma
kwenda Jijini Dar es Salaam aliposimama katika kijiji hicho baada ya kuona
wananchi wengi wakiwa wamekusanyika kando ya Ofisi ya Kata.
Baada ya kusimamisha msafara wake, Rais Magufuli aliwaita
wananchi waliokuwa wamekusanyika huku wakiwa wameshika mabango yaliyoandikwa
ujumbe wa kutaka wafugaji wa jamii ya Wamang’ati waondolewe na kisha akatoa
nafasi kwa baadhi yao kueleza dukuduku lao.
Wananchi hao ambao ni wakulima na mfugaji mmoja aliyejitokeza
wakaeleza kuwa Wamang’ati wamekuwa wakiwanyanyasa kwa kuingiza mifugo katika
mashamba yao ya mazao na wakithubutu kuwakataza wamekuwa wakichapwa viboko na
baadhi kuuawa.
Katika majibu yake, pamoja na kutaka wote wanaodaiwa
kuwashambulia wananchi kwa viboko wakamatwe Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa
Wilaya ya Bagamoyo kukomesha mara moja vitendo vya wafugaji kuwapiga wakulima
na wakulima kuwapiga wafugaji, na pia kukomesha vitendo vya wafugaji kulisha
mifugo yao katika mashamba ya wakulima.
“Kuanzia leo isitokee mfugaji kumpiga mkulima, mkulima kumpiga
mfugaji wala mfugaji kulisha mifugo yake kwenye mashamba ya wakulima na suala
hili nitalifuatilia mimi mwenyewe,” alisema. “Kwahiyo Mkuu wa Wilaya na
Viongozi mlishughulikie hili kabla mimi sijawashughulikia nyinyi, wale
waliopiga watu, nataka wote wakamatwe na wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.”
0 comments:
Post a Comment