RAIS MAGUFULI AAGIZA WENYE VYETI FEKI KUFUTWA KAZI MARA MOJA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza Waziri mkuu Kassim Majaliwa pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Angela Kairuki  kuhakikisha kwamba watumishi wote waliogundilika wakitumia vyeti feki wanaondoka katika maeneo yao ya kazi mara moja mwezi huu kabla hawajaadhibiwa kwa mujibu wa sheria.
Rais Dkt John Pombe Magufuli akihutubia katika ukumbi wa Chimwaga Dodoma wakati wa kupokea ripoti ya uhakiki wa vyeti feki
Rais Magufuli ameyazungumza hayo alipokuwa akipokea ripoti ya zoezi la uhakiki wa vyeti feki mjini Dodoma katika ukumbi wa Chimwaga, zoezi limefanywa kwa takribani miezi sita na waziri wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Angela Kairuki ambapo watumishi takribani 9932 wamegundulika wakitumia vyeti feki huku wengine 1538 wakitumia cheti kimoja kwa zaidi ya mtu mmoja.
“Watumishi 9932 wenye vyeti vya kugushi na feki mishahara yao ya mwezi huu ikatwe na waondoke kazini mara moja na hizo nafasi zitangazwe ili wasomi waweze kuziomba na majina yao yawekwe kwenye magazeti ili wajulikane” amesema Rais Magufuli
Rais Dkt John Pombe Magufuli  akipokea ripoti ya uhakiki wa watumishi waliogushi vyeti 
Pia amewataka wakuu wa idara kuhakikisha kwamba hadi kufikia tarehe 15 Mei 2017 watumishi hao wanaondoka na atakayekaidi agizo hilo atachukuliwa hatua za kisheria. Katika ripoti hiyo watumishi 1538 wanatumia cheti kimoja kwa zaidi ya mtu mmoja ambapo Rais ameamuru watumishi hao kutopewa mishahara mpaka watakapojulikana wamiliki halali wa vyeti hivyo na kuwataka watumishi wengine 11,769 kuwasilisha vyeti vilivyopungua.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Angela Kairuki amesema mpaka sasa vyeti vilivyohakikiwa ni 435,000, ambapo zoezi hilo l imefanyika kwa awamu tatu likijumuisha Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma, Tume na Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi na Wakala wa Serikali pamoja na Serikali Kuu.
“Leo tunakabidhi taarifa ya awamu mbili iliyohusisha Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma, Tume na Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi na Wakala wa Serikali ambapo imejumuisha uhakiki wa vyeti vya Kidato cha  Nne, Sita, vyeti vya ualimu kwa ngazi ya cheti na stashahada” amesema Waziri Kairuki.

Amesema kuwa matokeo ya uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa umma yapo ya aina nne ambapo watumishi 376,969 sawa na asilimia 94.23 wanavyeti halali, watumishi 9932 asilimia 2.4 wanavyeti vya kugushi, watumishi 1538 asilimia 0.3 vyeti vyao vinatumika kwa zaidi ya mtu mmoja na watumishi 11,769 asilimia 2.8 wanavyeti pungufu.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment