MAJALIWA; HAKUNA KIJIJI KITAKACHOKOSA UMEME

Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema hakuna kijiji kitakachokosa kuwekewa umeme katika mradi wa umeme vijijini wa awamu ya tatu REA III (Rural Energy Agency), kauli hiyo ameitamka leo alipokuwa akizungumza na wananchi wa jimboni kwake Ruangwa mkoani Lindi.
Waziri mkuu amesema serikali imetenga jumla ya Shilingi Trilioni moja kwa ajili ya kukamilisha usambazaji wa umeme katika vijiji 8,000 ambavyo mpaka sasa bado havijaunganishwa na nishati hiyo ya umeme.
Waziri MKUu Kassim Majaliwa akihutubia wananchi wa jimboni kwake Ruangwa mkoani Lindi
Waziri mkuu Kassim Majalwa yuko mkoani Lindi kwa ziara ya kikazi ya siku nne ambapo katika ziara yake aliyoifanya leo aliambatana na mkewe Mama Mary Majaliwa aliyasema hayo katika mikutano aliyoifanya kwenye vijiji vya Chiapi, Nandanga, Mbecha na Luchelegwa,
Mhe. Kassim Majaliwa ameongeza kwa kusema kuwa kwa sasa mwananchi hatowajibika na kulipia nguzo kwa ajili ya kuwekewa umeme nyumbani kwake bali atalipia Shilingi 27,000 tu. Kwa kutambua umuhimu wa huduma hiyo waziri mkuu Kassim Majaliwa amesisitiza kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha vijiji vyote vinafikiwa na nishati ya umeme na kwa vijiji ambavyo viko mbali na gridi vitafungiwa sola jambo ambalo litafungua fursa za ajira kwa wazawa.
Kwa upande wake Meneja wa Tanesco Mkoa wa Lindi Mhandisi, Johnson Mwigune  alimuhakikishia Waziri Mkuu kwamba hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu mkandarasi aliyepangiwa katika vijiji hivyo atakuwa tayari ameanza kazi ya kusambaza umeme.  
Mbali na hayo Waziri Mkuu amekabidhi gari kwa ajili ya kubebea wagonjwa jimboni kwake katika wilaya ya Ruangwa.
Waziri mkuu Kassim Majalia akikata utepe kuashiria makabidhiano ya gari ya wagonjwa kwa ajili ya Hospitali ya wilaya ya Ruangwa
Waziri Mkuu Kasim Majaliwa akikagua gari ya wagonjwa aliyoikabidhi kwa ajili ya hospitali ya wilaya ya Ruangwa. 


Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment