Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mhandisi Hamad Masauni, amelitaka Jeshi la Polisi kumuondoa katika nafasi ya
Mkuu wa Polisi, Usalama Barabarani (RTO) Mkoa wa Pwani na kuchukuliwa hatua za
kinidhamu kutokana kwa kushindwa kusimamia sheria za usalama barabarani mkoani
humo.
Masauni
akiwa ameambatana na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamishna
Msaidizi Mwandamizi, Fortunatus Musilimu, alitoa agizo hilo katika Kituo cha
Mabasi cha mjini Kibaha Maili Moja baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kituoni
hapo leo, kwa ajili ya kufuatilia maelekezo yake aliyoyatoa alipofanya ziara
kama hiyo mwaka jana.
“Mwaka
jana nilipofanya ziara kituoni hapa nilitoa maelekezo nilipokuta kuna mapungufu
katika ukaguzi wa magari, tukakubaliana atayafanyia kazi haraka iwezekanavyo,
lakini hakuna mabadiliko yoyote, magari hayakaguliwi, huku ni kuhatarisha
usalama wa abiria,” alisema Masauni na kuongeza kuwa;
“RTO
ameshindwa kuendana na kasi ya awamu ya tano, nataka aondolewe katika nafasi
hiyo na achukuliwe hatua ya kinidhamu, hatutati uzembe, hatutaki kucheza na
maisha ya watanzania.”
Masauni
mara baada ya ukaguzi wa kituo hicho, aliendelea na ziara yake mkoani Pwani
ambapo alifanya ukaguzi wa aina hiyo mjini Chalinze na baadaye Msata na
kuimalizia ziara yake Bagamoyo.
Akiwa
mjini Chalinze, Masauni alizungumza na waendesha bodaboda na kuwapa maelekezo
kuhakikisha wanafuata sheria za usalama barabarani kwa kutobeba mishikaki,
uvaaji wa kofia ngumu na pia kufuata sharia zote za usalama barabarani.
“Mmenihakikishia
kwa wale ambao hamkua na kofia ngumu kuwa mkitoka hapa mtakwenda kuzitafuta,
hakikisheni mnafanya hivyo kwa usalama wenu pamoja na abiria mnaowabeba,
ipendeni kazi yenu kwa kuheshimu sharia za usalama barabarani,” alisema
Masauni.
Akiwa
njiani kuelekea Chalinze mpaka Bagamoyo, Masauni ambaye gari yake ilitolewa
namba zinazomtambulisha nafasi yake (NWMNN), na kuweka namba za kawaida ili
kujua kama akiendesha kwa mwendokasi barabarani matrafiki watalisimamisha gari
lake, hata hivyo askari wa usalama barabarani sehemu kubwa hawakuwepo
barabarani na pia waliokuwepo hawakuweza lisimamisha gari lake.
Kutokana
na hatua hiyo, Masauni akagundua kuwa kuna uzembe mkubwa unaofanywa na
matrafiki mkoani humo kwa kutofanyakazi zao kwa umakini, na kwa uzembe huo ndio
chanzo cha ajali zinazotokea barabarani mara kwa mara.
Akizungumza
na matrafiki wilayani Bagamoyo ambao walifanya uzembe huo, aliwataka wabadilike
haraka iwezekanavyo kufuata wajibu wao, na pia alitoa siku tatu kuhakikisha
wanawakamata waendesha bodaboda wote ambao wanavunja sheria za usalama
barabarani, na pia baada ya operesheni hiyo apewe ripoti haraka iwezekanavyo,
na muda wowote atafanya ziara ya kushtukiza kuona kama maelekezo hayo
wameyafanyia kazi.
“Bodaboda
nimeziona nyingi zinapita hapa zikiwa zinavunja sheria, madereva na abiria
hawajavaa kofia ngumu, na nyie mpo hapa mnaziangalia, sasa nawaagiza mtekeleze
maagizo niliyotoa na pia sio nyie tu bali nchi nzima wahakikishe wanayakagua
magari pamoja na bodaboda, na atakaepuuza atutacheka nae, tutapambana nae,” alisema
Masauni.
Kwa
upande wake Kamanda Msilimu, alisema ameyapokea maagizo yote na atahakikisha
anayafanyia kazi ipasavyo kwa kuwasimamia matrafiki wote nchini kwa umakini
mkubwa.
0 comments:
Post a Comment