SERIKALI YATOA TAHADHARI KUHUSU UGONJWA WA TAUNI



Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa tahadhari kwa wananchi, kuhusu kuwepo ugonjwa wa tauni katika nchi ya Madagascar kuanzia Agosti, 2017.

Taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) imeeleza kuwa nchini Madagascar mikoa 8 imeripoti kupata wagonjwa ikiwa ni pamoja na Antananarivo ambao ni Mji mkuu wa Madagascar, Sava, Tamatave/Atsinanana na Majunga /Boeny. Kati ya Agosti 23 hadi Septemba 28 mwaka huu, wagonjwa 104 wameripotiwa na kati yao ishirini (20) wamepoteza maisha (CFR 19.2%).
Wagonjwa wengi walioripotiwa wameonesha kuwa na uhusiano kwa njia moja au nyingine na mgonjwa wa kwanza, jambo linalothibitisha kuwa yapo maambukizi ya ugonjwa wa tauni kati ya binadamu na binadamu. Hivyo, kwa mujibu wa WHO, upo uwezekano wa kadri (moderate risk) wa ugonjwa huo kusambaa katika nchi jirani na Madagascar.
Serikali imesema kuwa ahadhari hii inatolewa kwa kuzingatia kwamba nchi ya Madagascar haiko mbali sana na Tanzania, na inawezekana kukawa na muingiliano kati ya wananchi wa Tanzania na wale wa Madgascar. Inasisitizwa kwamba kwa sasa hapa nchini Tanzania hakuna mgonjwa yeyote aliyeripotiwa.
Aidha serikali imesisitiza kuwa mpaka sasa ugonjwa wa tauni haujaingia hapa nchini. Kwa kuwa magonjwa hayaangalii mipaka, tunahitaji kuchukua tahadharii madhubuti ili kuzuia ugonjwa huu usiingie hapa nchini. Hivyo wananchi wanahimizwa kuzingatia kanuni za afya za kuzuia ugonjwa huu, pia wanatakiwa kuripoti haraka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mara waonapo dalili zozote za ugonjwa huu.
Ugonjwa huu unasababishwa na bakteria anayejulikana kitaalam kama “Yersinia pestis”, ambaye hupatikana katika baadhi ya wanyama wadogo kama vile panya, paka na mbwa na viroboto. Njia kuu tatu ambazo mtu anaweza kupata maambukizi ni, Kung’atwa na viroboto vyenye maambukizi ya bakteria hao kutoka kwa wanyama kama mbwa na paka ambao huweza kubeba viroboto hawa. Kugusana bila kuwa na vikinga mwili na majimaji yenye vimelea vya bakteria kutoka kwa mtu/mnyama aliyeathirika kwa njia ya kugusa sehemu zenye vimelea zilizochafuliwa na mgonjwa/mnyama na kasha mtu huyo kujigusa mdomomi au puani. Kugusana na majimaji yanayotoka kwa mgonjwa kwa njia ya kukohoa au kupiga chafya bila ya mgonjwa huyo kufunika pua au mdomo.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment