Faru maarufu kwa jina John, ambaye alikufa
mwaka jana, alikufa akiwa katika hifadhi ya Sasakwa Grumeti kwa kukosa matunzo
na uangalizi wa karibu, kulingana na ripoti ya uchunguzi inavyosema.
Uchunguzi huo ulioongozwa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof.
Samwel Manyele uligundua kuwa kulikuwa na mapungufu katika kumtunza mnyama huyo
kabla ya kufa kwake
Prof Manyele amesema miongoni mwa mengine, hakukuwepo na kibali
rasmi cha kumhamisha Faru John.
Aidha, hakukuwa na mkataba wa kupokelewa kwa Faru John hifadhi
ya Sasakwa Grumeti na afya na maendeleo ya Faru John baada ya kuhamishwa
haikufuatiliwa.
Prof Manyele alisema hayo alipowasilisha ripoti ya uchunguzi kwa
Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa.
"Sababu za kifo chake zilichangiwa na kukosa matunzo na
uangalizi wa karibu, kukosa matibabu alipoumwa, mazoea yanayotokana na
kutofuata taratibu zilizowekwa kisheria na mapungufu ya kiuongozu kwa Wizara
husika, hifadhi na taasisi zake," alisema.
Maabara iliyotumika ni ya Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini
chini ya usimamizi wa timu ya wataalamu kutoka Tanzania, wachunguzi wa
Serikali, chini ya Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Prof Manyele amesema tume yake ilifanya uchunguzi wa kifo cha
Faru John kwa kupima vinasaba vya sampuli mbalimbali vikiwemo mzoga, fuvu,
mifupa, pembe, damu, ngozi na kinyesi kilichokaushwa ambapo ilibainika kuwa
vyote ni vya mnyama mmoja, aina ya faru mweusi ambaye ni dume.
Waziri Mkuu aliiunda tume hiyo Desemba 10, mwaka jana baada ya kupokea
pembe mbili za faru John na taarifa yenye nyaraka zilizotumika kumhamisha faru
huyo.
Hatua hiyo ilifuatia agizo alolitoa Desemba 6, 2016, akiwa
ziarani mkoani Arusha, ambapo alitoa siku mbili na kuutaka uongozi wa Mamlaka
ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote zilizotumika kumhamisha
faru John kutoka kwenye hifadhi hiyo.
Alitoa agizo hilo alipotembelea ofisi za makao makuu ya NCAA
zilizoko wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha na kuzungumza na watumishi wa
mamlaka hiyo pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya ziara
yake ya kikazi mkoani humo.
0 comments:
Post a Comment