Hosni Mubarak,
rais wa zamani wa Misri aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi na kupinduliwa mnamo
mwaka 2011 katika mapinduzi ya umma, ameachiwa huru kutoka kizuizini baada ya
miaka sita
Mwanasheria wa Mubarak Farid al-Deeb ameliambia gazeti binafsi
la al-Masry al-Youn kwamba Mubarak amerejea katika makazi yake yaliyoko katika
kitongoji cha Heliopolis, Mashariki mwa mji wa Cairo baada ya kuachiwa kutoka
hospitali ya kijeshi ambako alikuwa akizuiliwa. Kulingana na afisa usaalam wa
Misri, Mubarak aliondoka kwenye hospitali ya kijeshi iliyopo Cairo mapema
asubuhi ya leo. Alielekea nyumbani kwake akiwa chini ya ulinzi mkali. Mubarak
alirejea nyumbani akiwa na watoto wake wawili, Alaa na Gamal, na baadae
kuungana pamoja na familia yake nzima ikiwa ni pamoja na mkewe Suzanne.
Mubarak alikamatwa mwezi Aprili, 2011, ikiwa ni miezi miwili
baada ya kuondoka madarakani, na tangu hapo amekuwa akishikiliwa gerezani na
hospitali hiyo ya kijeshi akiwa chini ya ulinzi mkali, kwa tuhuma za kuagiza
mauaji ya waandamaji wakati wa uasi wa umma uliyosababisha kuangushwa kwake.
Wakati akishtakiwa kwa makosa hayo, tayari alikuwa ametumikia
kifungo cha miaka mitatu kwa makosa ya matumizi mabaya ya fedha za serikali.
Mnamo mwezi May mwaka 2015, mahakama ya uhalifu iliamua kumfunga kwa miaka
miatu jela na kumpiga faini ya Mamilioni ya Pauni za Misri kufuatia kosa hilo
la matumizi mabaya ya fedha zilizoainishwa kwa ajili ya ukarabati wa makazi ya
rais. Mahakama nyingine ilithibitisha hukumu hiyo mwaka 2016.
Mapema mwezi huu, mahakama ya juu ya rufaa ya nchini Misri
ilitoa hukumu ya mwisho iliyofuta makosa ya Mubarak mwenye umri wa miaka 88 ya
mauaji ya waandamanaji katika vuguvugu la mageuzi lililohitimisha utawala wake
uliodumu kwa miaka 30. Mubaraka amekuwa kizuizini tangu mwaka 2011. Makundi
mawili ya majeshi ya usalama yalisafisha njia kutoka hospitali hadi nyumbani
kwake, amesema mmoja wa afisa wa usalama kwa sharti la kutotajwa jina kwa kuwa
hakuwa na ruhusa ya kuzungumza na vyombo vya habari. Wanaharakati hata hivyo
wanasema, kuachiwa kwa Mubarak kutokana na makosa ya mauaji ya waandamanaji
kunathibitisha hisia zilizodumu kwa muda mrefu kwamba kesi yake pamoja na
askari polisi wanaokabiliwa na mashtaka ya kesi hiyo hayataweza kuleta haki
waliyoidai.
Raia wengi wa Misri waliokuwepo wakati wa utawala wake
walikichukulia kipindi hicho kama cha kilio, utawala wa mabavu na ubepari
uliohusisha maafisa wa serikali kushirikiana kwa karibu na wafanyabiashara
katika njia ya upendeleo. Waarabu walionesha kufurahishwa wakati picha
zinazomuonyesha kamanda huyo wa zamani wa jeshi la anga zilipoonyeshwa moja kwa
moja kwenye televisheni, akiwa amefungwa kitandani kwenye kizingo cha chumba
cha mahakama.
Kuangushwa kwa Mubarak, mmoja wa msururu wa wanajeshi
waliotawala Misri tangu kukomeshwa kwa utawala wa kifalme mnamo mwaka 1952
kulibeba matumaini uasi wa umma katika mataifa ya Kiarabu uliotikisa watawala
wa kimabavu kuanzia Tunisia hadi Ghuba na kwa muda mfupi kuibua matumaini ya
enzi mpya ya demokrasia na haki za kijamii.
0 comments:
Post a Comment