Timu ya Taifa
Stars ya Tanzania kesho inaingia uwanjani kucheza na Botswana kwenye Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam katika mechi ya kirafiki ya kimataifa katika wiki ya
kalenda ya FIFA.
Kwa umuhimu wa mchezo huo na hamasa ambayo uongozi wa Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania umeona hivyo TFF imeshusha bei ya kiingilio kwa watu
watakaokaa mzunguko kutoka Sh 5,000 hadi Sh. 3,000.
“Wavutieni Watanzania wakaishangilie timu yao, wekeni viingilio
vya bei ya chini ambayo Mtanzania itamweka katika mazingira ya kuchangia
gharama kidogo kwa timu. Toeni hiyo Sh 5,000 yenu. Wekeni angalau Sh. 3,000,”
ameagiza Rais wa TFF, Jamal Malinzi.
Pamoja na punguzo hilo kwa mashabiki wa mpira wa miguu
watakaoketi Majukwaa Maalumu – VIP “A” watalipia Sh 15,000 na wale watakaoketi
VIP “B” na “C” watalipia Sh 10,000.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Salum Mayanga kwa upande wake
aliwathibitishia Waandishi wa Habari kwamba kikosi chake kiko imara kwa ajili
ya mchezo huo utakaofanyika kuanzia saa 10.00 jioni.
“Tuna morali wa hali ya juu,” alisema Mayanga ambaye aliteuliwa
kuinoa timu hiyo mapema mwaka huu.
Kwa upande wa Peter Buffler Kocha Mkuu wa Botswana, alisema
kwamba anatarajiwa mchezo wa kesho utakuwa mgumu kwa sababu amegundua kuwa
kikosi cha Taifa Stars kina vijana wengi ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Mbali ya mchezo huo wa kesho, Taifa Stars inatarajiwa kucheza
mchezo mwingine dhidi ya Burundi Jumanne ijayo, Machi 28, mwaka huu. Mchezo
ambao pia ni wa kirafiki wa kimataifa unatarajiwa kuanza saa 10.00 jioni.
0 comments:
Post a Comment