Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, imemtaka msanii Agnes Gerald maarufu kama Masogange (28),
anayekabiliwa na kesi ya kutumia dawa za kulevya, kuheshimu masharti ya dhamana.
Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbroad Mashauri, alitoa rai hiyo Jumanne
hii baada ya video queen huyo kutokuwepo mahakamani wakati shauri hilo
lilipopelekwa kwa kutajwa.
Awali, Wakili wa Masogange, Nictogen Itege alidai mshitakiwa
huyo alikuwa njiani akija mahakamani hapo.
Hata hivyo, hakimu alimhoji wakili huyo mbona yeye (Itege) yuko
mahakamani hapo, ambapo alimjibu walipita njia tofauti na Masogange.
Baada ya kueleza hayo, hakimu Mashauri alimweleza wakili huyo
amwambie mteja wake anatakiwa aheshimu masharti ya dhamana.
Upande wa jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Aldof Mkini,
ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri hilo liahirishwe hadi tarehe
nyingine kwa kutajwa. Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 20, mwaka huu
kwa kutajwa.
Muda mfupi baada ya kuahirishwa kwa shauri hilo, Masogange
alionekana mahakamani hapo.
Masogange ambaye amejizoelea umaarufu nchini kutokana na kupamba
video za wasanii anakabiliwa na mashitaka mawili ya kutumia dawa za kulevya
aina ya Heroin na Oxazepam.
Katika kesi hiyo namba 77 ya mwaka 2017, Masogange anadaiwa kuwa
kati ya Februari 7 na 14, mwaka huu, katika maeneo yasiyojulikana ndani ya jiji
la Dar es Salaam alitumia dawa za kulevya aina ya Heroin (Diacety Imophine).
Pia anadaiwa kati ya Februari 7 na 14,2017 alitumia dawa za
kulevya aina ya Oxazepam.
Masogange aliposomewa mashitaka hayo kwa mara ya kwanza alikana
na upande wa jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika.
Hakimu Mashauri alimtaka mshitakiwa huyo kuwa na wadhamini
wawili wanaoaminika ambao kila mmoja atatia saini dhamana ya sh. milioni 10 na
asitoke nje ya jiji la Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali cha mahakama.
Masogange alifanikiwa kutimiza masharti hayo ya dhamana, hivyo
aliachiwa huru kwa dhamana hadi kesi hiyo ilipotajwa Jumanne hii.
0 comments:
Post a Comment