Malawi imetangaza kujiondoa kwenye
michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2019 pamoja na michuano ya Ubingwa
Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani ya 2018. Maamuzi hayo yamechukuliwa kutokana na
matatizo ya kifedha pamoja na kukosa kocha wa timu ya taifa. Shirikisho la Soka
la Malawi lilitoa taarifa baada ya kunyimwa idhini ya kumwajiri kocha kutoka
nje na serikali ya nchi hiyo.
Shirikisho la nchi hiyo lilitaka kumwajiri mkufunzi kutoka nje
ya nchi ambaye angelipwa mshahara kwa ubia wa nusu nusu kati ya shirika hilo na
serikali. Baada ya mashauriano ya miezi kadhaa, serikali kupitia Wizara ya
Michezo ilikataa pendekezo la shirikisho hilo kwa misingi ya kifedha na ndipo
kama tendaji ya shirikisho hilo ilipofikia uamuzi wa kujiondoa kwenye michuano
hiyo ya ubingwa wa bara la Afrika.
Timu ya taifa ya Malawi itaondoka rasmi kutoka kwa CHAN kufikia
31 Machi na kutoka AFCON kufikia 30 Aprili. Timu ya taifa ya Malawi ilikuwa imepangiwa
kucheza dhidi ya Madagascar mechi yao ya kwanza ya kufuzu kwa CHAN 2018,
michuano ambayo imepangiwa kuanza Aprili.
Kadhalika, walipangiwa kucheza nyumbani mechi yao ya kwanza ya
kufuzu kwa AFCON 2019 na mshindi wa mechi kati ya Comoro na Mauritius tarehe 13
Juni.
Malawi imekuwa bila mkufunzi wa timu ya taifa tangu Septemba
2016 raia wa Burundi Nsanzurwimo Ramadhan alipowaongoza kwa mechi moja ambayo
walishinda 1-0 dhidi ya Swaziland mechi ya kufuzu kwa AFCON alikuwa amechukua
usukani baada ya kufutwa kwa Ernest Mtawali Julai mwaka huo.
0 comments:
Post a Comment