Mkuu wa mkoa wa
Dar es Salaam amedaiwa kuwatishia kuwafunga jela miezi 6 au kuwapa tuhuma za
dawa za kulevya bila kupitia mahakamani wafanyakazi wa kituo cha utangazaji cha
Clouds Media Group kwa kukataa kurusha habari aliyoitaka
Waziri Nape Nnauye (kulia) akipokea taarifa ya uchunguzi kutoka kwa mwenyekiti wa Kamati, Hassan Abas |
Hayo
yamebainika katika ripoti ya uchunguzi wa tukio la kuvamia katika kituo cha
utangazaji cha Clouds lililofanya na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam akiwa na
askari wenye silaha, ripoti ambayo pia imependekeza mamlaka husika kumchukulia
hatua za kinidhamu.
Akiwasilisha ripoti hiyo kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo mbele ya wanahabari katika ukumbi wa Habari Maelezo jijini Dar es
Salaam, Mwakilishi wa Kamati ya uchunguzi Deodatusi Balile amesema kamati hiyo
haikuweza kumpata Paul Makonda kwa ajili ya mahojiano.
Akitaja mambo yaliyobainika katika sakata hilo, Balile amesema
kamati hiyo iliyohoji watu mbalimbali wakiwemo wafanyakazi 14 wa kituo cha
Clouds, imejiridhisha pasipo shaka kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul
Makonda alivamia katika kituo hicho saa 4:30 usiku wa Machi 17 akiwa anaendesha
gari yenye namba za usajili T553 BFH.
Amesema uchunguzi wa kamati umebaini kuwa sababu ya uvamizi huo
ni habari iliyodaiwa kumuhusu mwanamke aliyedai kuzaa na Mchungaji Josephati
Gwajima ambapo alitaka habari hiyo iruke kwenye kipindi..
Pia kamati hiyo imethibitisha kuwa Makonda na askari waliingia
hadi katika vyumba ambavyo hawakupaswa kuingia, na waliingia hadi kwenye studio
ambayo inarusha matangazo na kutoa vitisho kwa watangazaji, waandaji na
wafanyakazi wengine, kiasi cha baadhi yao kuagua vilio.
“Vitisho hivyo ni askari wenye silaha za moto, kuingia ndani ya studio
kibabe wakiwa na silaha za moto, Makonda aliwatisha usiku huo kwamba
angewafunga jela miezi sita, pia angewakagua watangazaji wa kipindi kama
wanahusika na dawa za kulevya, au kuwabana wadhamini wa kipindi na pengine
kuwaingiza kwenye orodha ya wahusika wa dawa za kulevya endapo wangeendelea na
msimamo wao” Amesema
Balile
Deodatus Balile akisoma taarifa hiyo |
Pia amesema kamati imebaini kuingiliwa kwa uhuru wa habari kinyume cha sheria kwa kulazimisha kutangazwa kwa habari isiyokidhi vigezo.
Kuhusu wafanyakazi kupigwa, Balile amesema kamati hiyo haikuona
uthibitisho wowote kuwa kuna watu walipigwa, isipokuwa wapo waliolia kutokana
na vitisho vya kupelekwa jela miezi 6.
Kamati hiyo imetoa mapendekezo manne ikiwa ni pamoja kumtaka
Makonda aombe radhi kwa tasnia ya habari, kumtaka Waziri kuwasilisha malalamiko
kwa mamlaka yake ya uteuzi ili hatua zichukuliwe, vyombo vya dola vianzishe
uchunguzi wa ndani dhidi ya askari walioingia.
Amesema kamati hiyo ilijirisha kuwa Makonda hakuwa tayari
kuhojiwa wala kutumia fursa ya kujieleza jambo ambalo hata hivyo
halikuathiri uchunguzi wa kamati hiyo.
"Tulianza kwa kumpigia simu, lakini hakupokea, tukaamua kumpelekea
ujumbe hakuujibu, tukatumia wasaidizi, wakatutaka tufike ofisini kwake,
tulifanya hivyo, tulifika lakini ilielezwa kuwa ana mgeni, ulipofika muda
akatuita, tukaelekezwa kupita ngazi za mbele lakini yeye akapita mlango wa
nyuma akaondoka. Tukaambiwa tumsubiri, tukasubiri lakini baadaye tukaambiwa
amepata shughuli nyingine kwa hiyo hataweza kurejea ofisini".
Amesema Balile
Waziri Nape akizungumza (kushoto) akiwa na Deodatus Balile |
Mara
baada ya kupokea ripoti hiyo, Waziri Nape amesema ataifikisha katika mamlaka
husika kwa ajili ya hatua kuchukuliwa huku akiwataka wanahabari kuendelea kuwa
na imani na serikali katika kulinda uhuru wa habari.
"Juu yangu kuna Waziri Mkuu, kuna Makamu wa Rais na kuna Rais,
nitawakabidhi ripoti hii, nawaomba wanahabari, tuendelee kuwa watulivu, Rais
wetu Magufuli ana nia njema na tasnia ya habari na ndiyo maana akaipitisha haraka
sheria inayoipa hadhi tasnia hii... Wakati mwingine madhaifu yakitokea kwa
mtendaji mmoja mmoja, yasiwe tope kwa serikali nzima....Mimi nitaipeleka
taarifa kwa wenzangu, wataiangalia na litakuwa ni funzo kwa watu wengine" Amehitimisha Waziri Nape
0 comments:
Post a Comment