Mwandishi wa habari na mtangazaji,
Maulid Kitenge, ambaye juzi alimnusuru aliyekuwa Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye dhidi ya mtu aliyemshikia bastola
wakati akielekea kuzungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya Protea,
jijini Dar es Salaam, amefunguka na kueleza kile kilichomsukuma aingilie kati.
Juzi, mara baada ya Nape kuwasili karibu na hoteli hiyo, ambayo
inapakana na Kanisa la Mtakatifu Petro, lililoko eneo la Oysterbay, aliposhuka
tu ghafla kijana huyo mrefu mweusi akiwa amevalia suruali ya jinzi, shati la
mikono mirefu la mistari mistari pamoja na kofia, alimkimbilia na kumshika mkono
kiongozi huyo akimtaka arudi kwenye gari.
Nape hakukubaliana na hatua hiyo, ambaye alimtaka kijana huyo
aonyeshe kitambulisho, lakini hakufanya hivyo, zaidi alirudi hatua chache nyuma
na kisha kutoa bastola iliyokuwa kiunoni kwake na kumtishia.
Wakati tukio hilo likitokea, ghafla alitokea kijana mwingine
aliyekuwa amevalia suruali na fulana nyeusi akimsaidia yule aliyekuwa ameshika
bastola kumsukuma Nape, ili arudi kwenye gari lake.
Ni katika mazingira kama hayo, ndipo waandishi wa habari
waliokuwa ndani ya Hoteli ya Protea wakimsubiri Nape walipoanza kusogea, huku
Mwandishi wa habari mashuhuri wa michezo nchini, Kitenge, akiwahi kufika na
kwenda moja kwa moja katika eneo ambalo Nape alikuwa akisukumwa aingie ndani ya
gari lake.
Kitenge alimsihi kijana huyo aache kumsukuma Nape na
alipoonekana kubisha aliamua kumsukuma pembeni.
MTANZANIA Jumamosi jana lilizungumza na Kitenge, ambaye alisema:
“Niliona mtu anamtolea Nape bastola nikashangaa, kwani muda
mfupi uliopita alikuwa waziri na isitoshe ni mbunge, sasa yule mtu aliambiwa
ajitambulishe, lakini hakujitambulisha,” alisema.
Alisema tukio lile lilimshtua, kwani mtu huyo aliyekuwa ameshika
bastola alikuwa akitetemeka sana, huku jasho likimtoka.
“Hatukumwelewa, kwanza hakutoa kitambulisho,” alisema Kitenge,
ambaye juzi wakati akimwokoa Nape alisikika akimwambia kijana huyo aliyeshika
bastola; “unaharibu bwana mwache, mwache bwana….”
Wakati tukio hilo linatokea walikuwapo waandishi wa habari
wachache, huku wengi wao wakiwa ndani ya hoteli hiyo wakimsubiri Nape, lakini
purukushani hizo ambazo ziliambatana na kelele ziliwashtua na hivyo kulazimika
kukimbia kuelekea eneo la tukio.
Waandishi wa habari walivyofika wengi mtu huyo hakuweza
kuonekana tena na ndipo Nape alifanikiwa kuzungumza nao.
Tukio hilo la kutolewa bastola lilitanguliwa na lile la Meneja
wa Hoteli ya Protea, aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Suleiman, kutangaza
kuzuia mkutano wake na waandishi wa habari usifanyike katika hoteli hiyo, kwa
kile alichodai kuwa, ni maelekezo kutoka kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kinondoni, Susan Kaganda.
Source; MTANZANIA NEWSPAPER
0 comments:
Post a Comment