Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.
January Makamba ameagiza kusitishwa mara moja kwa shughuli zote za kibinadamu
kando kando ya Vyanzo vya maji.
Rai hii imetolewa leo na Waziri Makamba mara baada ya kufanya
ziara ya kukagua hali ya mazingira katika Mkoa wa Pwani eneo la Mto Mpiji ambao
umeathirika kutokana na Uchimbaji wa mchanga na mmomonyoko wa ardhi unaohatarisha
maisha ya wakazi wa eneo hilo.
Waziri Makamba amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo
Bi. Fatuma Latu kuwaondoa watu wote waliojenga pembezoni mwa Mto Mpiji na
kuhakikisha zoezi hilo linafanyika ndani ya siku 30. " Mkurugenzi
hakikisheni kuwa wakazi hao waliovamia eneo la mto huu na kujenga makazi yao ya
kudumu wanaondolewa mara moja" Alisisitiza Waziri Makamba.
Katika hatua nyingine Waziri Makamba ametembelea Mto Wami na
kusikitishwa na uharibifu mkubwa wa mazingira unaosababishwa na shughuli za
kibinadamu ikiwa ni pamoja na kilimo, ufugaji na uchimbaji haramu wa madini,
upasuaji mbao na uchomaji mkaa unaopelekea mmomonyoko wa udongo na
mchafuko/tope jingi na kusababisha kupungua kwa uzalishaji wa maji.
Katika kukabiliana na changamoto zilizoainishwa Waziri Makamba
amesema Ofisi yake itaanda kikao kazi kitakachojumuisha wadau wote muhimu ili
kunusuru Mto Wami haraka iwezekanavyo. "Serikali haiwezi kuwekaza fedha
nyingi kwenye mradi mkubwa kama huu na kuona uharibifu ukiendelea na kuharibu
miundombinu, hali hii haikubaliki na nitachukua hatua za haraka” alisema waziri
Makamba.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano
na Mazingira), Mhe. January Makamba (Mb.) yuko katika ziara ya kikazi katika
mikoa Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Singida kujionea hali ya
mazingira na changamoto za hifadhi katika mikoa husika.
Waziri wa nchi ofisi ya makamu wa rais (Muungano na mazingira) Mhe. January Makamba alipotembelea mamlaka ya usafi na mazingira Chalinze |
Moja ya nyumba ambazo zinatakiwa kubomolewa kutokana na kujengwa ndani ya mita sitini kutoka katika chanzo cha maji. |
0 comments:
Post a Comment