WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amewaomba viongozi na wananchi wa Tanzania Bara na Visiwani
kushirikiana kwa pamoja katika kuimarisha na kuulinda Muungano ulioachwa na
waasisi wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
Ametoa
kauli hiyo leo (Ijumaa, Aprili 7, 2017) mara baada ya kushiriki hitma na kuzuru
kaburi la Sheikh Karume lililoko Afisi Kuu za Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Kisiwandui mjini Unguja wakati wa maadhimisho ya kifo cha Rais wa kwanza wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Sheikh Abeid Karume sambamba na
siku ya Mashujaa Zanzibar
Amesema ni
muhimu kwa wananchi kutenga muda wao na kuwaombea viongozi wetu waliotangulia
mbele ya haki, lengo likiwa ni kukumbuka na kuenzi mchango mkubwa waliotoa
katika kujenga msingi wa maendeleo ya Taifa.
Waziri Mkuu
amesema Watanzania wote Bara na Visiwani ni wamoja kiasili, hivyo wanapaswa
kushirikiana katika kudumisha misingi iliyoachwa na waasisi wa Taifa ili kuweza
kujiletea maendeleo
Pia
amewaomba Watanzania wote kuhakikisha wanashirikiana kwa pamoja kuulinda na
kuudumisha Muungano ulioachwa na waasisi wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere
na Sheikh Karume.
“Tuhakikishe
Muungano huu tulioachiwa na wasisi wa Taifa letu unadumu ili tuendelee kuwa
wamoja na kuzungumza lugha moja ya kuboresha maendeleo na kulinda amani na
utulivu wa nchi yetu,” amesema.
Aidha,
Waziri Mkuu amesema katika kutambua umuhimu wa viongozi hao Serikali imetenga
siku maalumu kwa ajili ya maadhidhimisho ya vifo vya viongozi hao na kutoa
fursa kwa wananchi kila mtu kwa imani yake kuwaombea dua na kutafakari namna
walivyojitoa kwa taifa letu.
Maadhimisho
ya kifo cha Sheikh Karume ni Aprili 7 ya kila mwaka na Hayati Mwalimu Nyerere
ni Oktoba 14 ya kila mwaka. Maadhimisho
hayo ya kifo cha Sheikh Karume yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali
wakiongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali
Mohamed Shein, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Pili wa Rais wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd.
Wengine ni
Rais Mstaafu wa awamu ya Pili, Sheikh Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa
Zanzibar, Dkt. Amani Abeid Karume, Makamu wa Rais Mstaafu Dkt. Mohamed Gharib
Bilal, wazee wa CCM pamoja na wananchi.
0 comments:
Post a Comment