DC HAPI AMALIZA MGOGORO SUGU WA ARDHI WILAYANI KINONDONI


Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Ally Hapi leo amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa maeneo ya Nakasangwe, Nakalekwa na kumaliza mgogoro wa ardhi uliodumu eneo hilo kwa miaka 13 na kusababisha vifo.
DC Ally Hapi
Hapi amesema kuwa ikiwa ni muendelezo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi wilayani Kinondoni  ofisi yake ilizikutanisha pande mbili za wenye mashamba na wakazi ambazo kwa miaka kadhaa zimekua kwenye mgogoro mkubwa na kufanya nao mazungumzo yaliyoweka msingi mzuri wa kumaliza mgogoro huo.
DC Hapi aliwaambia wakazi wa maeneo hayo kuwa upimaji wa viwanja utafanyika na wote waliohakikiwa watapewa viwanja vyao
"Tumeamua sasa eneo hili lote lipimwe viwanja, ili wakazi wote mliohakikiwa kila mmoja apate kipande cha ardhi cha kuishi na familia yake na viwanja vinavyobaki wapate wenye mashamba. Hii ndiyo njia pekee ya kuweza kuwafanya muishi kwa amani katika mji uliopimwa na kupangwa vizuri." Alisema DC Hapi
Aidha, Hapi aliwaeleza wananchi hao kuwa katika eneo hilo zaidi ya viwanja 6000 vitapatikana na hivyo kuwatoa shaka kuwa wakazi wote zaidi ya 3000 waliohakikiwa kila mmoja atapata ardhi iliyopimwa huku wenye mashamba nao wakipata viwanja vitakavyobakia ili waweze kuviendeleza au kuviuza vikiwa na hati miliki.
DC Hapi amesema kazi ya upimaji wa ardhi katika eneo hilo inatarajiwa kuanza haraka na kumalizika ndani ya kipindi cha miezi mitatu chini ya kampuni ya Afro Map ambayo pande mbili zimeichagua kufanye kazi hiyo.
"Nawapa kampuni hii miezi mitatu tu, kazi ya upimaji iwe imekamilika eneo hili ili wananchi wangu waishi kwa amani wakijua serikali yao ipo kuwasaidia." Alisema DC.
Mgogoro wa Nakasangwe ulianza mwaka 2004 na hivyo kudumu kwa miaka 13 kipindi ambacho kilitawaliwa na chuki, uhasama na uadui mkubwa baina ya wenye mashamba na wananchi waliovamia mashamba hayo. Watu kadhaa walipoteza maisha katika mgogoro huo.

Wananch wote wanaounda pande mbili za mgogoro wamemshukuru DC Hapi na kushikana mikono kama ishara ya mwisho wa mgogoro huo na mwanzo mpya.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment