Takribani wazabuni 66
kutoka ndani na nje ya nchi wamejitokeza kununua Nyaraka za Zabuni za
ujenzi wa mradi wa Umeme wa kiasi cha megawati 2100 katika maporomoko ya maji
ya Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) mkoani Pwani hadi kufikia tarehe 19 Septemba,
2017.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kamati ya kusimamia ujenzi wa
mradi huo, Mhandisi Leonard Masanja wakati wa mkutano na wazabuni hao
uliofanyika jijini Dar es salaam, Septemba 18, 2017. Mkutano huo ulilenga kutoa
maelezo mbalimbali kuhusu mradi kwa wazabuni hao.
Hata hivyo, Mhandisi Masanja aliweka wazi kuwa, Serikali bado
inaendelea na zoezi la kuuza nyaraka za zabuni hizo, ambapo tarehe ya mwisho ya
kuzirudisha kwa ajili ya kuzifanyia tathmini na kumpata mshindi wa zabuni
hiyo ni Oktoba 16, 2017.
Akieleza kuhusu mkutano na wazabuni hao ambao ni makampuni na
wakandarasi mbalimbali, Mhandisi Masanja alisema kuwa, wazabuni hao walipatiwa
maelezo hayo baada ya kutembelea eneo la mradi na kujionea hali halisi ya eneo
husika.
Aidha alisema kuwa, katika
mkutano huo, wazabuni hao walipata fursa ya kuuliza maswali na kueleza
changamoto mbalimbali walizoona kwenye eneo la mradi na katika nyaraka za
zabuni ambapo baadhi ya maswali yao yalijibiwa papo hapo na mengine kuandaliwa
na kusambazwa kwa wazabuni wote walionunua nyaraka za zabuni.
Agosti 30, 2017, Serikali kupitia Naibu Waziri wa Nishati na
Madini Dkt. Medard Kalemani ilitangaza zabuni ya kuanza ujenzi wa Mradi Mkubwa
wa Umeme wa megawati 2100 katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji mkoani Pwani
(Stiegler’s Gorge).
Dkt. Kalemani alifafanua kuwa tayari taratibu za awali
zilikwishaanza ambapo wataalam wa ndani na nje walishakutana na kuchagua
sehemu za kujenga mradi huo katika Mto Rufiji, Shirika la Umeme Nchini (TANESCO)
lilishaanza upembuzi yakinifu wa kujenga miundombinu ya kufikisha huduma umeme
katika eneo la mradi utakotumika wakati wa ujenzi na Wakala wa Barabara
nchini (TANROADS) kujenga miundombinu ya Barabara.
Sambamba na hilo, Dkt. Kalemani aliweka wazi kuwa mkandarasi
atakayepewa kazi ya kujenga mradi huo ni yule tu atakayeridhia kujenga mradi
kwa gharama nafuu na kwa muda mfupi ndani ya kipindi cha miezi 36.
Alisema kuwa tayari Serikali imetenga fedha za kutekeleza mradi
huo ambao unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu baada ya kumpata mzabuni
na kuanza ujenzi wake.
Mradi huo utakapokamilika utasaidia kuimarisha upatikanaji wa
huduma ya Umeme nchini.
0 comments:
Post a Comment