Serikali imesema ipo tayari kugharamia matibabu ya Mbunge wa
Jimbo la Singida Mashariki Tundu Antiphas Lissu ambaye kwa
sasa hivi yupo Jijini Nairobi kwa matibabu kufuatiwa shambulio alilolipata
Septemba 7, mwaka huu Mkoani Dodoma.
Hayo yamesemwa Jijini Tanga na Waziri wa Afya,Maendeleo ya
Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akiongea na waandishi wa habari
kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
Waziri Ummy Mwalimu alisisitiza kwa kusema kuwa Serikali
inasubiri kupata maombi kutoka kwa familia ya mgonjwa ikiambatana na taarifa
rasmi kutoka kwa madaktari kuhusu mahitaji ya matibabu zaidi ya
mgonjwa ”Serikali ipo tayari kugharamia matibabu zaidi ya Mhe.Lissu
popote Duniani” alisema Waziri Ummy. Aliongeza kwa kusema, akiwa kama Mtanzania
na Mbunge,Serikali inayo wajibu wa kugharamia matibabu yake hadi apone ili
aweze kuendelea na kazi ya kuwahudumia Watanzania na wana Singida Mashariki.
Aidha, Serikali imeshangazwa na dhana ya kuchangishana kwa
ajili ya matibabu ya Mhe. Lissu, kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kutokea
matapeli watakaochangisha Watanzania fedha kwa madai kwamba Mbunge huyo amekosa
hela za matibabu.
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto
anawashukuru Madaktari na watoa huduma wote wa Hospitali ya Rufaa Dodoma kwa
kazi kubwa na nzuri waliyoifanya katika kuokoa maisha ya Mhe.Lissu na kumtakia
apate nafuu haraka.
0 comments:
Post a Comment